Wednesday, July 24, 2013

NA SAADA AKIDA

Abdallah Kibadeni
WAKATI ratiba ya Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza rasmi Agosti 24, mwaka huu ikionyesha vigogo wa soka nchini, Simba na Yanga wataumana Oktoba 20, kocha mkuu wa Simba, Abdallah 'King' Kibadeni amesema kwa sasa hataki kusikia habari za Yanga.

Badala yake amewataka wanachama na washabiki wa timu hiyo, kumuacha ili atengeneze timu ya kudumu itakayoiletea mataji ya ndani na nje klabu yao.

Akizungumza na DIMBA, Kibadeni alisema katika usajili aliousimamia msimu huu, amelenga kuandaa wachezaji vijana ambao wataweza kucheza vizuri na kwa muda mrefu.

Alibainisha kuwa hata usajili wake wa wachezaji kutoka nje ya nchi, ulizingatia umri na uwezo wa mchezaji, lengo likiwa ni kupata wachezaji wa kudumu.

Kibadeni ambaye msimu uliopita aliiwezesha timu ya Kagera Sugar aliyokuwa akiinoa kushika nafasi ya nne, msimu huu aliibukia Simba na kuanza kuendesha usaili na pia kujaribu wachezaji kadhaa kutoka nje ambao baadhi yake wamesajiliwa na wengine wametupiwa virago.

Juzi kocha huyo alithibitisha kumsajili beki wa URA ya Uganda, Joseph Owino ambaye pia aliwahi kuzichezea timu za Simba na Azam FC kwa nyakati tofauti na kisha kumtupia virago beki mwingine raia wa Uganda, Samuel Ssenkoom.

Simba inatarajia kuanza kampeni yake ya kuwania taji la Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, Agosti 24, mwaka huu kwa kuivaa timu iliyopanda daraja msimu huu, Rhino Rangers ya Tabora, katika mchezo utakaofanyika katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora.

Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

0 comments:

Post a Comment