Wednesday, July 24, 2013

NA SAADA AKIDA

KOCHA Mkuu wa Kagera Sugar, Mganda Jackson Mayanja amesema hana presha na Ligi Kuu Tanzania Bara, hasa baada ya kupangiwa kuanza ligi ugenini dhidi ya Mbeya City, lakini ikicheza pia mechi ya pili ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar.

Akizungumza na DIMBA jana, Mayanja alisema hana presha na mechi hizo ingawa hatadharau mchezo wowote kwani ili kupata mafanikio mwisho wa ligi ni lazima kufanya vizuri kwenye mechi za mwanzo pia.

“Siwezi kuidharau timu yoyote kwenye ligi, lakini ninachokifahamu ni kwamba Mbeya City ni timu ngeni katika ligi, lakini imejiandaa na ligi kwa kiwango kikubwa kwa hiyo tutaendelea kupambana kuhakikisha kwamba tunapata matokeo mazuri mwisho wa msimu. 

“Nafurahia kwa sababu ligi tumeanzia ugenini na wenzetu watakuwa kwenye uwanja wa nyumbani, lakini hiyo ni changamoto ya kuendelea kufanya vizuri kwenye ligi hasa kwa mechi za kwanza, naelewa kuwa ni jambo ambalo linawezekana,” alisema Mayanja raia wa Uganda.

Katika ufunguzi wa ligi hiyo, Agosti 24 mwaka huu, Kagera Sugar itaanza na Mbeya City huku Yanga ikiwa mwenyeji wa Ashanti United mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, lakini Simba ikianzia ugenini dhidi ya Rhino mjini Tabora.

0 comments:

Post a Comment