Wednesday, July 24, 2013


RATIBA ya michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyotolewa juzi, inaonyesha timu zilizopanda daraja msimu huu, Ashanti United ya jijini Dar es Salaam, Mbeya City ya jijini Mbeya na Rhino Rangers ya Tabora, zitafungua dimba na timu vigogo katika ligi hiyo.

Ligi hiyo inayotarajiwa kuanza Agosti 24, kiasi cha mwezi mmoja ujao, itazikutanisha timu za Yanga na Ashanti, katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.

Timu ya Rhino ya Tabora, itaikaribisha Simba katika uwanja wake wa nyumbani wa Ali Hassan Mwinyi uliopo mjini humo.

Timu ya Mbeya City inayotajwa kuwa na washabiki wengi mkoani humo, itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wake wa nyumbani, Sokoine mjini Mbeya.

Ukiangalia ratiba hiyo tu, utaona jinsi timu hizo zinavyotakiwa kujiandaa vizuri ili ziweze kuanza michuano hiyo kwa kuwapa matumaini washabiki wake.

Tunafahamu jinsi wachezaji wanaoanza kucheza michuano ya ligi kuu wanavyokuwa na taharuki, hasa wanapocheza na wenzao waliobobea kwenye michuano hiyo, lakini tunazishauri timu hizo kujiandaa na kisha kushiriki bila woga.

Tunanawashauri makocha wa timu hizo, kuacha kuwafundisha soka la uwanjani pekee wachezaji wake, bali pia wakumbuke umuhimu wa kuwajenga kisaikolojia ili wawe kujina sawa na wachezaji wenzao wawe wa Simba, Yanga au Azam.

Endapo wachezaji wa timu hizo watajitambua na kisha watajiona kama washiriki halali, basi kutakuwa na uwezo wa kuishuhudia ligi ya msimu huu ikiondoa 'ufalme' wa kudumu wa soka la Tanzania kwa timu za Simba na Yanga.

Hata hivyo tunazitakia kila la kheri timu zote zinazoshiriki ligi hiyo, ziwe na maandalizi mazuri yatakayoleta tija katika soka la Tanzania.

Tunazitambua changamoto zilizotawala soka letu, hasa udhamini usiotosheleza mahitaji, lakini yote hayo tumeyazoea na ndiyo tunayoendelea kuyashuhudia hivyo basi suala la jitihada nalo lipewe nafasi ili kuleta mapinduzi hayo.

Next
Newer Post
Previous
This is the last post.

0 comments:

Post a Comment